Mh Rais Nakusalimu .
Wakati mwingine unapaswa kupewa pole na kuombewa na kufanyiwa dua kwani wewe
ndie unatumikia ofisi kubwa kuliko zote Nchini na wakati huo huo unapaswa
kupewa hongera kufikia malengo yako hayo ya kutumikia ofisi kubwa na ya Heshima
kuliko zote Nchini , nimekuwa nikitafakari sana suala la Udini katika Taifa
letu na huko Nyuma mwaka jana nilikuandikia pia waraka kuonya na kukumbusha
hatua mathubuti kabla mambo hayajaaribika sijui kama ulisoma lakini naamini
Usalama wa Taifa ambao siku hizi wanatumikia CCM watakuwa walisoma na Nape na
wenzake pia walipata fursa ya kuusoma .
Mh Rais katika waraka hule nilisema hivi “ Mh Rais Taifa linahitaji Tiba “
siwezi leo kuandika kile nilichosema katika waraka ule ila niliweza kubashiri
sumu ya udini inayoendelea katika Taifa lako na
langu, Mh Rais , ukweli nakwambia ukifanya mchezo kidogo sana Taifa hili
linapotea likiwa mikononi mwako kwani hali ya Nchi sio nzuri hata kidogo na
watu waliokuwa wanaishi kwa umoja na upendo sasa wanaanza kutafuta mbinu za
kugombana na kuuwana.
Mh Rais, Siasa ya Udini na Ukanda makusudi yake yalikuwa kudhoofisha vyama vya
upinzani na yalifanikiwa kwa baadhi ya vyama kudhoofishwa sana na mkakati huo
unaendelea dhidi ya Chadema lakini kinachosikitisha ni kuwa wale waliobuni
mkakati huo walishindwa kutafakari au kuona madhara yake mbele .
Mh Rais, mkakati wa kudhoofisha Chama cha Siasa kwa Udini na Ukanda
hauishi tu kuangamiza hicho Chama bali kuwagawa Watu na Taifa kwa Ujumla
, Mtu anapojaribu kusema Chadema ni Chama cha Wakristo kimsingi matamshi
hayo hayaangamizi Chadema tu bali yanagawa Watu kwa matabaka ya Udini wao na na
kufanya Dini moja iamini kuwa Dini nyingine ni mbaya na hivyo mpango huo
unafanya Watu waanze kutazamana kwa Udini na Ukabila na matokeo yake ndiyo haya
tunaanza kuyaona leo .
Mh Rais, Taifa linahitaji tiba , Hivi karibuni Waziri Mkuu alienda Geita kwenye
mgogoro wa Waisilamu na Wakristo na niliona mawazo ya Waziri Mkuu kwenye
vyombo vya habari na kwa kweli nilisikitika kwa
busara zile zilizokuwa zimejaa hofu kubwa . Tatizo lile lilianza na nani kati
ya Mkristo na Muislamu anayepaswa kuchinja?
Mh Rais , Nilipoona jambo hili nilianza kujiuliza maswali mengi sana, kwanza ,
umakini huu kwa pande zote mbili juu ya jambo hili umeletwa na nini na
nani? Kwani yako mambo mengi yaliyokatazwa na Biblia na Msaafu ambayo watu wote
wa dini hizi mbili wamekataa kuyatii au kuyafuata , kwa mfano waislamu na
wakristo vijana kwa wazee wanakunywa pombe pamoja baadhi yao kujenga
mahusiano hata ya kimapenzi yasiyo rasmi bila hata kufuata
utaratibu wa Msaafu wala Biblia lakini hapa hutaona ugomvi mkubwa sana
japokuwa ni masuala yanayo mkera na kumuudhi mwenyezi Mungu sana.
Mh Rais , ndio maana katika suala hili la nani achinje kati ya Muislamu na
Mkristo niliposikia maafa yake nikakumbuka waraka niliokuandikia mwaka
jana kuhusu choko choko za Udini ambazo zimeanza
kuleta maafa ambazo Mwanzilishi wake ni CCM .
Mh Rais Chama chako unachokiongoza , Team yako imekuwa ikifanya sana
propaganda hizi za, Udini , Ukabila , na Ukanda usiku na mchana , lakini
nimekuwa nikikerwa sana na Jinsi kabila la Wachaga
linavyochukuliwa katika propaganda hizi na wanaofanya hivyo asilimia kubwa ni
mashemeji wa Wachaga na mimi najiuliza wanaweza vipi kufanya Siasa za Ukanda na
Ukabila wakati wao wenyewe ni familia moja ?
Kwa mfano , Mh Mwigulu Nchemba , Mh David
Mathayo , Mh January Makamba , Mh Benjamin Mkapa , Mh Fredrik Sumaye , Mh Theo
, Mh Dr Faustin Ndungulile , Mh Prof Ibrahimu Lipumba , Pro Mahalu
, Mh Dr Hamis Kigwangala , Mh John Mgufuli , Mh Sospeter Muhongo , Mh
Jaji Warioba, Idd Simba, Mh Salmin Amour , na wengine wengi wote hawa wameoa
Kilimanjaro . Sasa unajiuliza hawa wote ni Viongozi ndani ya CCM na wengine
ndio mabingwa wa kufanya Siasa za Udini na Ukanda , je wake
zao ndani ya nyumba wanajisikiaje wanapoona waume zao wanatukana kabila za
ndugu zao kwa sababu ya Siasa ? Hii ni hatari kubwa Mh Rais kama kuchinja ni
suala zito kiasi hicho katika Imani ya Kiislamu na pia ni neno kutoka katika
Kitabu cha Imani yao basi ni haki na kweli kuwa wao wanapaswa kuchinja
kwa Imani ya Dini yao na wala wasilazimishwe kumkosea Mungu wao kwani hakuna
maarifa na Busara
inayozidi imani, lakini vile vile Wakristo wasilazimishwe kushiriki Ibada
ambayo sio yao. Waislamu kama wanaamini kuwa wao kuchinja ndio jambo
lililoamrishwa katika vitabu vyao basi sasa Jambo hilo liheshimiwe na
kutafutiwa utaratibu na vile vile Wakristo wasipuuzwe kugoma kushiriki jambo
ambalo kwa wengine lina sura ya Imani.
Nini Kifanyike?
Kwanza Chama chako na Viongozi wake uwakanye na kuwashauri mara moja kabisa
kuacha propaganda za udini na ukanda , kwani katika hili hakuna namna
Nchi inaweza kubaki salama , kwani hizo choko choko hazitokani na nia mbaya ya
Waislamu na Wakristo bali ni siasa chafu iliyopandikizwa ili kuangamiza vyama
vya Siasa na sasa imekwenda zaidi na imeanza kuwatesa wakati ambao Nchi ina
matatizo mengi , Kwa mfano Chadema tulipoandama Arusha kupinga Uchaguzi wa Meya
feki ,
Kiongozi mmoja wa Mkoa wa CCM hapa Arusha , alinukuliwa na vyombo vya
habari akidai tunafanya maandamano hayo kwa sababu za Udini na ndio maana
hatumtaki Meya , lakini kitu cha kushangaza huyu Meya Feki ni Mkristo
tena Mchaga Kabila langu , lakini niliambiwa na tunampinga na Maaskofu
wanampinga kwa sababu Chadema ni Chama cha Udini ‘ sasa najiuliza kama
Meya huyu Feki ni Mchaga na ni Mkristo je hayo madai ya kijinga
yanatoka wapi ? Kama Ukristo ni ajenda kubwa kwetu kwani
nini tulimpinga sasa ? Huu ni mfano mmoja iko mingi sana inayoashiria mkakati
wa makusudi wa kuangamiza Chadema na huku mkisahau kuwa maliangamiza Taifa
, na ndio Mkuu wa Mkoa wa Arusha alipokuja tu alidai kuwa amekuja
kupambana na Chadema na Wachaga , ila nimuhakikishie hataweza na asijaribu
kamwe na mikutano ambayo amekuwa akiifanya aiche mara moja .
Pili, Mh Rais, ninaamini kuwa wewe umesafiri Nchi mbali mbali kuliko mimi ,
Ukienda Marekani , Spain , Brazil , China , Hong Kong , UK, Italy , Sweden,
Botswana , Namibia , South Afrika , Zimbabwe na Nchi
nyiongi utaona Maduka au Mabucha ya Nyama yameandikwa (Halal ) au unanua
bidhaa yeyote ya aina ya Nyama na kukuta imeandikwa “Halal” na ni ustarabu
kwamba bidhaa hiyo machinjio yake yamezingatia maadili ya Dini ya Kiislamu na
Waislamu wenye Imani thabiti na Imani yao hapo ndipo watakapofanya manunuzi
yao katika bidhaa hiyo ya aina ya Nyama. Lakini maeneno hayo hayo unaweza
kupata nyama katika maduka mbali mbali yasiozingatia utaratibu huo na kwa
hivyo watu wasiojali sana
masuala ya Imani wala hawatasumbuka kuuliza na kusoma kama Nyama hiyo
imezingatia masuala ya matakwa ya Imani Fulani.
Hivyo, Mh Rais, nafikiri ni vyema utaratibu
huu ukaletwa hapa kwetu ili tuonyeshe Kujali Imani ya Waislamu katika Jambo
hili ambalo limekuwa kwazo katika Jamii hizi mbili kubwa na kama ufumbuzi wake
hautakuwa kuzingatia hili basi tarajia uchungu kuendelea kutembea kwenye vifua
vya watu bila kusema na siku moja hali inaweza kuwa mbaya na tukapoteza Taifa.
Mh Rais, naiona hofu isiyokuwa ya kweli ya Mh Waziri Mkuu kuwa tukiruhusu
hilo kuwa Wakristo na Waislamu wataweza kutengana kwenye mambo mengine mengi
haswa katika Biashara na mambo mengine , kitu ambacho nasema sio kweli
kwani , Sukari ,Mchele , Soda na Juisi na bidhaa nyingi hazina makatazo na
maelekezo katika Imani , Mfano kila Mkristo anajua kuwa Mwislamu hatumi Nguruwe
na Nguruwe kwa mwislamu ni haramu na hivyo Mkristo hawezi kupika Nguruwe na
huku akijua kuwa
wageni wake siku hiyo ni Waislamu.
Kwa hiyo hofu ya kuligawa Taifa kwa kurusu
jambo hili haliwezi kutokea kwani ni miiko ya Kiimani ambayo pande zote
zinapaswa kuheshimiana ili upande mmoja usione umekandamizwa na kupuuzwa , na
hofu ya kibiashara inayoweza kutokea katika suala hili inapaswa kupuuzwa kwani
IMANI ni zaidi ya Biashara japokuwa sioni jambo hili likitokea .
Mh Rais, nisikuchoshe sana, lakini haya ni maoni yangu na Mke wangu na
sio Chama changu tumeamka leo Asubuhi tukasema tukuandikie tena kwani wewe ni
Mkuu wa Nchi , Najua unaweza kuwa busy sana kusoma waraka huu mrefu ila najua
Mwigulu na Nape lazima wausome na Rizwan pia hivyo niwaombe wakufikishe ujumbe
huu kwa niaba ya familia yangu.
Mh Rais , We are pressed on every side by troubles, but not crushed and broken.
We are perplexed because we don,t know why things happen as they do . But we
don’t give up and quit, we are hunted down BUT God never abandons Us, We get
knocked down BUT we get up again and keep going. The root of life need
commitment and there’s a lot of suffer to get at the Climax. Don’t Give Up
Mr President please, Help our Country now.
Godbless Jonathan Lema

ni kweli kabisa kamanda, lema
ReplyDelete