Sisi Watanzania
wapigania maendeleo - CHADEMA UK tumelazimika kuwasilisha majonzi yetu kwenu
kwa njia hii, ikiwa ni katika kuonyesha mshikamano wa kitaifa kwa kujifariji na
pia kuwafariji ninyi waTanzania wenzetu kutokana na tukio kubwa la kuhuzunisha
sana ambalo limetokea hivi majuzi nchini mwetu huko mkoani Arusha.
Pamoja na kwamba
pamekuwa na matukio kadhaa yaliyoikabili nchi yetu hili la Arusha tumeonelea
tulisemee kwa njia ya kipekee, kwa sababu licha ya kwamba ni tukio la kigaidi,
lisilokuwa na mantiki yeyote ile zaidi ya umwagaji damu wa raia wasio kuwa na
hatia, bali pia utekelezwaji wake unaweza kutuachia athari kubwa sana
kisaikolojia na kimahusiano kama tusipojaribu kulitathmini na kulitafakari kwa
upekee wake.
Wakati ambapo sala
na maombi yetu kwa sasa yawaeendee wafiwa na wale ambao wamedhurika moja kwa
moja kimwili ama kisaikolojia kutokana na tukio hili, tunapenda pia kupongeza
juhudi zilizofanywa na kila mmoja wetu aliyeweza kuwafikia na kutoa msaada wa
aina moja ama nyingine kwa wahanga wa janga hili bila kujali tofauti ya vyama,
itikadi, kabila, dini ama falsafa. Hiyo ndiyo Tanzania tunayoijua sisi. Pamoja
na tofauti zetu nyingi ki hali,afya ama kipato, lakini kamwe hatubaguani katika
misingi ya rangi, kabila ama dini. Na hili ndio haswa linalotusukuma sisi
kuwasilisha huu waraka wa rambirambi kwenu ninyi wenzetu leo hii.
Tuna imani kwamba
vyombo vyetu vya usalama vitafanya utafiti wa kina kuchimbua na kutujuza chanzo
cha ufedhuli huu, ni lazima sisi wenyewe pia tufarijiane kwa maombi, michango
na tafakuri mbalimbali zenye kutiana moyo katika kipindi hiki kigumu kwetu
sote. Tuna imani kwamba yeyote aliyehusika katika mkakati huu atapatikana na
kupewa adhabu inayostahili.
Kwetu sote
Watanzania, huu ni wakati muafaka kuonyesha mshikamano wetu kuwatumia ujumbe
hao wachache wenye nia mbaya kwamba Watanzania tumeundwa kutoka jumuiya ya
makabila zaidi ya mia moja, wenye asili, rangi, dini na madhehebu mbalimbali na
wasioamini. Na kati yetu wote sisi ni marafiki na ndugu, wengine ni ndugu wa
damu kabisa, kupitia ndoa, wazazi n.k. Hivyo sisi hatuwezi kubaguana wala kuwa
na chuki miongoni mwetu kwani hiyo si asili yetu. Na yeyote yule atakayejaribu
kupandikiza mbegu hii chafu miongoni mwetu tumkatae na kumchukilia hatua stahiki
kumtokomeza yeye na kundi lake.
Ujumbe wetu kwa
Watanzania ni huu:
HII NI VITA DHIDI YA
UMOJA WETU WA KITAIFA NA SIYO KUNDI AU IMANI FULANI.
Asanteni sana, Mungu awabariki nyote. Mungu alibariki taifa letu
Tanzania.
Kwa niaba ya CHADEMA UK
G Mboya
Katibu

No comments:
Post a Comment