SIKU 47 nilizokaa jela, nimejifunza mambo mengi ambayo yamenipa hisia, hari na nguvu ya kupigania nchi yangu niwapo hai ili Watanzania waweze kupata mabadiliko ya haraka.”
Hiyo ni kauli ya Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Mkoa wa Dar es Salaam (CHADEMA), Henry Kilewo, ambaye alikamatwa na wenzake wanne kwa tuhuma za ugaidi.
Baadye shitaka hilo lilifutwa na kubakiwa na shtaka la kummwagia tindikali kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mussa Tesha. Waliachiwa kwa dhamana Agosti 7, mwaka huu.
Kilewo na wenzake, Avodius Justinian (Bukoba), Oscar Kaijage (Shinyanga), Rajabu Daniel (Dodoma) na Seif Magesa (Mwanza) wanatetewa na mawakili, Prof. Abdallah Safari na Peter Kibatala.
Siku aliyokamatwa
Kilewo anasema alipigiwa simu na maofisa wa polisi makao makuu Juni 17, mwaka huu, wakimwarifu kuwa wanataka kufanya mahojiano naye lakini hawakueleza yanahusu nini.
Anasema Juni 21, mwaka huu akiambatana na wakili wake, Peter Kibatala na John Mnyika (Mbunge wa Ubungo) walikwenda polisi makao makuu ili ahojiwe.
Kada huyu anasema akiwa huko, alihojiwa mambo mbalimbali likiwamo tukio la kummwagia tindikali Musa Tesha, jambo ambalo lilimshangaza.
“Nilicheka sana kwa kuwa kabla ya kuitwa nilipata taarifa za kikao kilichofanyika Dodoma ili kuniunganisha na kesi ya ugaidi…mahojiano yangu yalifanyika wakati tayari kuna kesi iliyokuwa inaendelea huko Igunga,” anasema.
Kilewo anasema baada ya mahojiano hayo na kuandikisha maelezo ilipofika saa 11:30 jioni, polisi walimnyima dhamana na kumpeleka rumande ya Kituo Kikuu cha Polisi.
Anasema Juni 22, mwaka huu, familia yake ilifika kumtembelea ikakatazwa, lakini baadaye wakili wake aliwasiliana na makao makuu ya polisi ndipo wakaruhusiwa kumuona.
“Siku hiyo hiyo usiku nilisafirishwa kwa ndege nikapelekwa Igunga kuunganishwa kwenye kesi ya kummwagia tindikali Musa Tesha, baada ya kukataa kujibu maswali ya kuwahusisha viongozi wangu na vitendo vya utekaji vinavyotokea nchini,” anasema.
Akiwa gerezani Uyui
Kilewo anasema alipoingia katika Gereza la Uyui alikuta kuna msongamamo mkubwa ambao ulichukua zaidi ya wiki moja. Wafungwa na mahabusu walimkaribisha kwa kumweleza matatizo yao.
Anasema kwa kuwa ni kiongozi, kila mtu alikuwa akimweleza yaliyomsibu kuingia gerezani humo na hata mateso yalimo.
“Katika hali ya kushangaza nilikutana na watu mbalimbali wa nchi jirani kama vile Congo, Burundi, Rwanda na Uganda ambao wamefungwa kwa tuhuma mbalimbali.
“Kwangu ilikuwa ni faraja kukutana na watu wa mataifa hayo ambao walinieleza ukweli kuhusu mambo mbalimbali, ikiwamo vita ya ukanda wa Maziwa Makuu inayoendelea na ndoto za hao wafungwa baadaye,” anasema.
Kilewo anasema kwa sasa hawezi kuizungumzia vita na maono ya mahabusu na wafungwa hao bali ataieleza katika kitabu chake anachoandaa kwa kushirikiana na wakili wake, Peter Kibatala.
Anasema kwa kushirikiana na wakili wake Kibatala pamoja na mkewe, Joyce Kiria, wataandika kitabu kitakachohusu siku 47 alizokaa jela, mateso na hali halisi zilivyo katika magereza na kuelezea kuhusu maono ya raia wa nje waliofungwa.
“Naweza kusema kidogo kuwa wengi wa mahabusu na wafungwa hawa wanasema kuwa waliingia kwa uonevu na kutokuwa na haki za binadamu gerezani humo,” anasema.
Kilewo anasema maneno aliyoelezwa na wenzake hayakuchukua siku kwani naye yalisikia mwenyewe kutoka kwa askari jela akimwamrisha mtu kufanya kazi huku akimweleza kuwa hakuna haki za binadamu.
Anasema neno hilo alilipinga waziwazi, akimtaka askari huyo amweleze sehemu ilipoandikwa kisheria kwamba hakuna haki gerezani.
“Toka siku hiyo askari huyo aliniwekea kinyongo na kuanza kuniogopesha mara kwa mara …sikutetereka hata kidogo, niliishi kwa ujasiri kama kiongozi,” anasema.
Anasema katika kumwonesha kuwa yeye ni nani alimweleza kuwa hatakubali kuonewa na kuwa mnyonge bali atatii na kufuata sheria zilizopo jela.
Aidha, anasema maisha gerezani humo ni magumuu lakini ilimbidi ayazoee ingawa kula na kulala ilikuwa tabu, ingawa alipewa fursa ya kula vizuri kwa manyapala ila aligoma na kuamua kushiriki na wenzake.
Anasema kwa nyakati tofauti kila mtu kwa wakati wake, walikumbana na mateso mengi likiwamo la kulazimishwa kuwataja viongozi wa juu wa chama chao, Mwenyekiti Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, John Mnyika na Tundu Lissu kuwa wanahusika na ugaidi.
Anasema askari watesaji walifikia hatua ya kuwalaghai kuwa watapewa vyeo serikalini na fedha ili mradi wawahusishe viongozi wa CHADEMA na ugaidi.
Aporwa ujumbe wa kumpa Mbowe
Kilewo anasema katika kudhihirisha kuwa askari wa gerezani wana uonevu, siku ambayo Mwenyekiti wake wa taifa, Freeman Mbowe, alipowatembelea akiwa na viongozi wengine, mara baada ya kumaliza mazungumzo alimpa ujumbe wa maandishi ili awape Watanzania.
Cha kushangaza akiwa anampa mkono, mmoja wa askari gerezani humo alimpora kijikaratasi hicho na kuhifadhi.
“Nilikasirika sana kuona nanyimwa haki ya kuwasiliana na kiongozi wangu … lakini ujumbe huu nilitaka uwafikie Watanzania, nilipotoka juzi niliuweka katika mtandao wa kijamii wa facebook na kupata wachangiaji zaidi ya 50 na wengine wanaendelea,” anasema.
Ujumbe wenyewe ni huu
“Kwa Watanzania wataka mabadiliko, jela si sehemu salama ya kuishi, wala haijawahi kuwa sehemu salama ya kuishi, wala haitakaa iwe sehemu salama ya kuishi pasipotokea wajasiri na wazalendo kama mimi na wewe kwenda kuishi kwa hiari sehemu ambayo utawala dhaifu wa CCM kama kitisho cha kuzuia mabadiliko. Watawala wabovu kwenye nchi yetu hutumia jela kama kitisho cha kuzuia ukweli, ukiruhusu kitisho cha kuogopa jela utakuwa mwanamabadiliko kigeugeu na mnafiki machoni mwa umma. Kitisho hiki kamwe sintokiruhusu mimi Henry Kilewo hata kwa mtutu wa risasi za moto, japokuwa natambua athari za kukaa jela muda mrefu kama ambavyo shujaa wa dunia Nelson Mandela anavyopitia kwasasa, hii kwangu ni sadaka tosha kwa taifa, chama, familia, ndugu jamaa na marafiki zangu. Ni onyo na funzo kwa watawala dhaifu kudhani wataweza kuzuia harakati hizi za mabadiliko kwa kuvitumia vyombo vya dola vibaya kama Usalama wa Taifa, Jeshi la Polisi, mahakama na hata magereza. Kamwe tusiruhusu kuwa wanyonge wala kukubali kuonewa kwani watatuzuia kwa muda, watatudhalilisha kwa muda na siogopi kukaa jela ila moyo wangu unasononeka pale nionapo saa ya ukombozi inachelewa. Ni muda tu, tutashinda.
Ujumbe kwa Jaji Warioba na Waziri Silima
Kilewo anasema akiwa gerezani aliaminiwa na wenzake hadi kumpa ujumbe mzito wa kwenda kwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Anasema wafungwa na mahabusu hao wanataka Jaji Warioba kama walivyowafuata kuwataka maoni na wao kuyatoa, kuiweka sheria itakayowawezesha kupiga kura, kwa kuwa ni haki yao ya msingi.
Katibu huyo anasema wafungwa hao wanataka iwe ivyo ili nao wawe mtaji wa wanasiasa ambao ni watetezi wa Watanzania na watunga sheria.
Pamoja na hilo, wanataka pia iwekwe wazi sheria ya jela na stahiki anazotakiwa kupata mahabusu na mfungwa kama binadamu na si hivi wanavyoishi sasa kama wanyama.
Pia wamemtaka kufikisha ujumbe wao kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Silima, kwamba wakiwa gerezani wanapata mateso makali na si kweli kwamba hakuna mateso kama alivyozungumza bungeni hivi karibuni.
Anasema wafungwa hao wamemtaka awaeleze kuwa kuna vyumba vya mateso vinavyoitwa Punishment Cello (PC), ambavyo vinatumiwa katika magereza mengi kuwatesa.
Wamemtaka pia ashughulikie suala la wao kupata nakala za hukumu na maombi mengine wanayoyatoa kwa wakati, waboreshewe majengo ikiwamo kuondoa msongamano, wawekewe vitanda, mashuka, sabuni mafuta na chakula.
Aidha, wanamtaka waziri huyo kutembelea magereza na kujionea hali halisi na si kuishia kwa wakuu wa jela ambao wakati mwingine wanamweleza mambo ya uongo.
Kilewo anasema ingawa aliishi katika mazingira magumu kama hayo, wenzake walimwona kama mfalme, kwani walimtumia vizuri, naye alieneza vema siasa ya mabadiliko.
“Namshukuru Mungu sasa nimerudi uraiani, kazi yangu ya kueneza siasa ya mabadiliko naendelea nayo kama kawaida … nipo Dar es Salaam, kesho kutwa naelekea jimboni kwangu Mwanga kwa ajili ya kuwasalimu wananchi wangu, mabadiliko ni lazima,” anasema.
Mke wa Kamanda Kilewo Joyce Katika mwenye watoto wawili

Hii kitu ni tamu sana... nami naihifadhi kwenye kumbukumbu zangu
ReplyDeleteKaka wewe ni soo, endelea tupo nyuma yako kwa hali na mali.
ReplyDelete