Social Icons

.

Saturday, 22 March 2014

TUCTA ya beza hutuba ya Rais Kikwete


SIKU moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kulifungua Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma, hotuba hiyo imebezwa na viongozi wa vyama vya wafanyakazi, wakidai amepuuza maoni ya Watanzania.
Walisema, hotuba ya mkuu huyo wa nchi imejaa siasa na kubeza kazi nzuri iliyofanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uenyekiti wa Jaji mstaafu Joseph Warioba.
Kwa nyakati tofauti, viongozi hao waliwataka wajumbe wa Bunge hilo wasusie mjadala huo kwa kuwa maoni ya wananchi kutaka muundo wa serikali tatu yamepuuzwa.
Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Mkoa wa Dodoma, Ramadhani Mwendwa, alisema hayo jana wakati akitoa maoni yake kwa mwandishi wa habari hizi mjini hapa, kuhusu hotuba ya ufunguzi wa bunge hilo.
Katika maoni yake, Mwendwa ambaye pia ni Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi ya Juu, Habari na Utafiti (RAAWU), Kanda ya Kati alisema kitendo cha Rais Kikwete kupuuza maoni ya Watanzania wanaotaka serikali tatu, kinakinzana na dhamira halisi ya taifa kupata katiba inayotokana na matakwa yao.
Alieleza kwamba kwa vile serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanataka muundo wa serikali mbili kinyume na matakwa ya wananchi wanaowaongoza ni wazi kwamba hata vitatumika vitisho kwa wananchi wakati wa kuipigia kura ya maoni rasimu hiyo baada ya kupitishwa bungeni.
“Msimamo wa serikali mbili kwa wananchi ni wa kulazimishwa na dola. Hii inatokana na kwamba dola haitambui raia wake kwamba wana haki ya kusikilizwa na kutimiziwa natakwa yao… inawezekana kabisa Rais Kikwete anaamini alichaguliwa kwa bahati mbaya.
“Halafu kama serikali mbili ni nzuri mbona Rais Kikwete ameshindwa kueleza uzuri na matatizo yake badala yake amezungumzia matatizo ya serikali tatu tu?” alisema Mwendwa.
Alimpongeza mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba na kusema: “Mzee Warioba kwa mawazo yake mazuri ya taifa hili… ana busara lakini baadhi ya viongozi ndani ya CCM na serikali ni mafisadi.”

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...