Social Icons

.

Monday, 8 October 2012

Utajiri wa gesi Tanzania ni kitendawili kwa wananchi kunufaika na utajiri huwo wa Asili

NAIKUMBUKA vizuri kauli ya wahenga inayosema penye miti mingi hapana wajenzi. Kauli hii ina ukweli ndani yake kutokana na taifa letu lilivyobarikiwa kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali za asili. Tanzania ni taifa ambalo limefanikiwa kuwa na utajiri mkubwa wa maliasili yakiwamo madini ya dhahabu, almasi,Tanzanite, makaa ya mawe, makaa ya chuma, gesi, mbuga za wanyama, ardhi kubwa na yenye rutuba na hali ya hewa nzuri. Taarifa za kiutafiti kutoka gazeti la New York Time lililopo nchini Marekani limebaini kwamba Tanzania ni nchi ya kwanza kwa vivutio barani Afrika na kwamba inashika nafasi ya tano Duniani. Pamoja na kuwapo kwa utajiri huo na ukilinganisha na miaka 50 tangu tupate uhuru, utaona ni vitu viwili visivyokuwa na uhusiano. Kampuni ya Pan African Energy Tanzania Ltd (PAT) ambayo iliingia mkataba na Serikali wa kuchimba gesi iliyopo Songosongo kwa gharama za uendeshaji kiasi cha dola 133 milioni za Marekani. Kampuni hiyo imechimba visima vitano kati ya visima vinane vilivyopo katika mgodi huo na kuzalisha futi za ujazo 105 milioni za gesi kwa siku. Sekta ya gesi nchini inatoa mchango kidogo tofauti na utajiri uliopo wa gesi hiyo katika ardhi ya kusini mwa nchi hususani maeneo ya mwambao na tafiti zinaeleza kuna utajiri wa gesi zaidi ya futi za ujazo 7 trilioni na kati ya hizo zilizothibitishwa ni 1.142 trilioni. Kwa utajiri uliopo katika Kijiji cha Songosongo ni futi za ujazo 2 trilioni na inahusishwa kutoa mchango wa megawatti 178 tu za umeme kupitia kampuni ya Songas inayozalisha. Utajiri mkubwa wa gesi hiyo inaonekana kutokuwa na faida yoyote ile kwa wakazi wa kusini na maeneo ya mwambao kwa kuwa wanaendela kuishi gizani kwa kipindi kirefu angali kuna chanzo kikubwa cha umeme. Utata mkubwa upo katika mkataba kati ya mwekezaji na Serikali, umetoa nafasi kubwa ya kimaslai kwa mwekezaji na kuwa na jeuri ya kuendesha mradi huo anavyotaka akijihakikishia uhalali wa kile anachokifanya. Kwa mujibu wa ukaguzi uliofanywa na Kamati ya Bunge kuhusu sekta ndogo ya gesi ilibaini kampuni hiyo inajiinufaisha kwa kutumia gharama zisizo halali—Sh46.3 bilioni na kusababisha Serikali kukosa gawio lake la dola 20.1 milioni za Marekani. Wakati huohuo kampuni hiyo ilishindwa kuthibitisha uhalali wa kurejesha gharama zake nyingine zinazofikia dola36 milioni za Marekani na kuendelea kuonyesha mashaka makubwa katika kuendesha sekta ya gesi. Hasara hizo zilizojitokeza kupitia mikataba mibovu, Serikali inaweza kuzifidia kwa njia ipi na kumrudisha Mtanzania kwenye hali ya uaminifu? Nasema hivyo kwa sababu zaidi ya dola 110 bilioni za Marekani zimesababisha shaka kupitia kampuni hii. Fedha hizo nikitumika kwenye sekta ya miundombinu, zinaweza kujenga barabara kwa kiwango cha lami zaidi ya kilometa 100 na upande wa elimu, fedha hizo zinaweza kutumika kujenga maabara na kuweka vitanda vya kutosha katika hosptali zetu. Kuhusu taarifa ya Zitto Kabwe bungeni kuhusu sekta hiyo, inafafanua kwamba, duniani kote zipo familia mbili za mikataba ya mafuta na gesi ambazo ni ‘Concessionary’ na ‘Production Sharing Agreement’(PSA) katika kuleta maslahi katika pande zote mbili yaani mwekezaji na Serikali. Mataifa makubwa duniani kama vile Marekani, Uingereza na Canada yanatumia mfumo wa ‘Concessionery’ na kampuni ya mafuta binafsi inapewa haki zote za mchakato wa kutafuta, kuchimba, kusafirisha na kuuza mafuta au gesi. Mfumo huu wa umiliki wa mafuta na gesi unakuwa chini ya kampuni na siyo Serikali na hivyo kampuni hiyo inalipa mirahaba na kodi zinazohitajika serikalini. Uchunguzi ulibaini kuwa mkataba uliopo kati ya TPDC na PanAfrican Energy Tanzania Ltd ni mbovu kuliko mikataba yote nchini kwani TPDC inalipa mrahaba wa asilimia 12 na katika huohuo mrahaba, kodi ya mapato hukokotolewa. Mkataba huu tulionao katika sekta ya gesi naufananisha na ule wa chifu Mangugo aliyetawala eneo la Msovero hapa nchini katika kipindi cha unyonyaji. Chifu Mangugo alisaini mkataba na Serikali ya Kijerumani uliokuwa unaeleza kutawala eneo lake pasipo kuelewa jambo hilo na kutafasiriwa kinyume na mkataba unavyosema kwa kuwa alikuwa hawezi kusoma kilichoandikwa katika mkataba. Naweza pia kutolea mfano wa Mtanzania aliyebadilishana dhahabu na kete kule Shinyanga bila kuona hasara yoyote. Serikali imeshindwa kusimamia sekta hii ili kuleta maslahi kwa Watanzania. Hali hii inaonyesha jinsi gani Serikali haikuwa makini katika kusaini mkataba wa kuendesha shughuli za kuchimba na kuzalisha gesi ya Songosongo kwa manufaa ya Mtanzania wa kawaida. Kutomnufaisha Mtanzania hususani mkazi wa anaishi au anayetoka kwenye maeneo yenye utajiri kama wa gesi, kumesababishwa na kukosekana kwa sheria ya gesi nchini jambo ambalo linasikitisha kuona utajiri unapotea. Endapo Serikali itasimamia ipasavyo kwa kutizama upya mikataba, kutunga sheria ya gesi na kuboresha mazingira ili kuvutia wawekezaji, na kutoa ajira kwa Watanzania wengi ambao hawana ajira. Uzalishaji wa gesi ukiongozeka, kampuni mengi yatashawishika kuingia makubaliano ya kununua umeme wa gesi na kuendelea kukuza uchumi wa Taifa letu. Mtanzania leo hii anatumia gesi kwa bei kubwa katika matumizi ya ndani kwa mfano, mlaji analazimika kununua mtungi wenye kilo 15 za gesi kwa Sh55,000 wakati gesi inazalishwa hapa nchini. Bei hiyo ni sawa na mtu anayenunua gesi kutoka nchi za nje kwa mfano China au Sngapore. Serikali inapaswa imiliki asilimia 70 mpaka 75 ya shughuli za kuchimba na kusafirisha gesi ili iweze kuwa na uwezo wa kuuza bidhaa hiyo kwa gharama nafuu kwa wananchi wake. Kama Serikali itaweza kumiliki sehemu kubwa ya mradi huo basi itafanikiwa kuhifadhi mazingira yetu kwani wataalamu wa hali ya hewa duniani wanasema gesi ni rafiki wa mazingira. Serikali ijaribu kufanya haraka katika kutekeleza ahadi yake ya maisha bora kwa kila Mtanzania ili kuondoa dhana ya maneno ya ulaghai katika kipindi cha uchaguzi.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...