Social Icons

.

Thursday, 17 April 2014

Matusi Bungeni yamuibua JK

RAIS Jakaya Kikwete amekemea vitendo vya wajumbe wa Bunge la Katiba kuwatusi waasisi wa taifa hili na kusema huo ni utovu wa nidhamu na ukosefu wa adabu. Katika mazungumzo yake na wahariri wa baadhi ya vyombo vya habari jijini Dar es Salaam juzi, rais alisema ni kukosa adabu kwa baadhi ya Watanzania kuwatukana, kuwadhihaki na kuwakejeli waanzilishi wa Tanzania, hayati Julius Nyerere na hayati Abeid Aman Karume. “Viongozi hawa wawili wameifanyia Tanzania mambo mengi makubwa na mambo ya kihistoria kiasi cha Watanzania kuona kwamba wanao wajibu wa kudumisha na kuenzi heshima yao kwa namna ya kudumu,” alisema kwa taharuki alipokuwa akizungumzia miaka 50 ya Muungano. “Ni kukosa adabu na ni utovu mkubwa wa nidhamu kwa Mtanzania yeyote kuwatukana, kuwadhihaki ama kuwakejeli waasisi wa taifa letu. Hawa ni watu ambao waliifanyia nchi yetu mambo makubwa. “Mzee Karume yule aliongoza Mapinduzi yaliyoondoa dhuluma na uonevu pale Visiwani. Waafrika walio wengi walikuwa wanaonewa sana pale, pengine watu wamesahau lakini hata pale walipokuwa wanashinda uchaguzi bado walikuwa hawapewi nafasi ya kuongoza maisha yao wenyewe. “Ni ukosefu wa adabu kwa yeyote kumshutumu mtu aliyejitolea kiasi hicho ili kubadilisha mfumo dhalimu na kujenga maisha na mazingira bora kwa wengi. “Mzee Nyerere ametuachia taifa moja, lililoungana, lenye umoja, amani na mshikamano. Misingi aliyoijenga imeendelea kuongoza taifa letu kwa miaka yote hii… “Viongozi wengine wote waliofuata kina mzee Mwinyi, mzee Mkapa na sasa mimi mwenyewe, tumefuata na kuongozwa na misingi hii,” alisema na kuongeza kwamba siku nchi yetu inaamua kuipuuza misingi hiyo tutaingia kwenye matatizo. Rais Kikwete alitoa msimamo huo baada ya kuulizwa kuhusu matusi, kejeli na dhihaka zinazoonyeshwa na wajumbe wachache wa Bunge Maalumu la Katiba juu ya waasisi wa Tanzania na wabunifu wa Muungano. Mwigulu amtaka afute uteuzi Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Mwigulu Nchemba, amemtaka Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta, kumwandika barua Rais Kikwete, atengue uteuzi wa wajumbe aliowateua kuingia kwenye Bunge hilo. Mwigulu alitoa akauli hiyo juzi jioni alipokuwa akiomba mwongozo mara baada ya wajumbe kutoka Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kutoka nje ya Bunge wakisusia mijadala kwa madai ya kuendeshwa kwa ubaguzi na matusi. Mwigulu, alisema kuwa baadhi ya wajumbe waliotoka nje kuungana na UKAWA ni wale wa kundi la 201 walioteuliwa na rais hivyo ni vema utaratibu ukafanywa kuangalia namna ya kuwaondoa bungeni. “Naomba uandike barua kwa rais atengue uteuzi wao, na ateue watu wengine ambao wapo wengi nje ya Bunge hili wanaohitaji kuja hapa ndani kutunga Katiba ya wananchi hata bila ya malipo,” alisema. Mwigulu alisema jambo hilo pia lingeweza kufanyika kwa wajumbe wengine ambao ni wabunge wa Jamhuri ya Muungano au Baraza la Wawakilishi lakini kwakuwa sheria inakuwa ngumu kwao, wanachi ndio wataamua. Mwigulu alidai kuwa UKAWA kwa muda mrefu walikuwa na mkakati wa kukwamisha mchakato wa Katiba lakini walikosa fursa ya kuanza kutekeleza jambo hilo. Alibainisha kuwa amesikitishwa na kitendo kilichofanywa na UKAWA ambao wana lengo la kuvunja muungano kwa kupitia hoja ya kutaka serikali tatu. “Mungu anaipenda nchi yetu, mchakato huu wa Katiba tunao hivi sasa kwa hekima ya rais wetu na bila ya yeye tusingekuwa na nchi inayoitwa Tanzania,” alisema. Mwigulu alisema tangu siku nyingi UKAWA wamekuwa wakifanya majaribio ya kukwamisha mchakato wa Katiba tangu Bunge lilipokuwa linatunga Sheria ya Katiba, wajumbe waliamua kutoka nje. Alisema wakati huo UKAWA walitoka nje na kutoa vitisho vingi vilivyowapa hofu wananchi na Rais Jakaya Kikwete akawasihi wakutane naye ili kuondoa tatizo hilo. Aliongeza kuwa baada ya kukutana na Rais Kikwete, hatua ya pili UKAWA walitoa mengine huku wakitoa vitisho vya kutumia helikopta zaidi ya tano kuzunguka nchi nzima kuwaelezea wananchi juu ya mchakato wa Katiba unavyovurugwa na CCM. “Jamani mtakumbuka kuwa Rais Kikwete wakati akilihutubia taifa kwa unyenyekevu aliwaomba wasifikie hatua hiyo bali wakutane wazungumzie tofauti zao, kwakuwa kila jambo linawezekana katika meza ya mazungumzo…rais wetu alifanya hivyo lakini wao hawakuonekana kujali,” alisema. Mwigulu aliongeza kuwa vituko hivyo vya UKAWA viliendelea katika kutunga kanuni ambapo walitaka ripoti kinzani iwepo katika usomaji, hali iliyozusha makubwa yaliyotishia kuvunjika kwa Bunge. Aliongeza kuwa walio wengi wakapata taarifa kuwa UKAWA wamepanga ikiwa hawatapewa taarifa kinzani wataharibu mchakato wa Katiba. Alibainisha kuwa UKAWA wakafanikiwa kupata nafasi ya kuwa na ripoti kinzani na walipokwenda kwenye ufafanuzi ambao ilipangwa ripoti ya wajumbe wote iwe saa moja, ambapo dakika 20 zitakuwa za wachache, ambapo hata hivyo walitaka dakika 30 za ufafanuzi, la sivyo watatoka nje. “UKAWA kwa hiyo wakawa na dakika 20 za taarifa yao kusomwa na 30 za ufafanuzi, hivyo walikuwa na dakika 50 huku tulio wengi tukiwa na dakika 40, ambapo tuliomba tuongezewe dakika 10 lakini ilishindikana,” alisema. Aliongeza kuwa UKAWA walizidi kuvutana kwa siku 40, kuhusu kura ya wazi na siri ambapo walikuwa wanataka ya siri huku walio wengi wakitaka ya wazi. “Tulipowakubalia UKAWA wapige kura ya siri wakaenda kupiga ya wazi na kuwalazimisha watu wao wapige ya wazi,” alisema. Alibainisha kuwa UKAWA, waliendelea kulisumbua Bunge baada ya kugomea uteuzi uliofanywa na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu kwa wajumbe wa Kamati ya Uongozi wakidai wengi ni kutoka CCM. “UKAWA walisema kama mwenyekiti hatawaondoa wale waliotaka waondolewe wao watajitoa na mchakato utaishia hapo, jambo ambalo mwenyekiti alikubali na kuwafuta ili kuruhusu mchakato uendelee,” alisema. Mwigulu alisema UKAWA walitafuta sababu nyingine ya kukimbia bungeni kwa kisingizio kuwa hati ya Muungano haipo na waliposikia hati ipo walishindwa kwenda kuwaandaa wananchi juu ya hati hiyo. “Niwaombe Watanzania pimeni wenyewe… kikanuni tumeweka Kamati ya Maridhiano ambayo jambo tusiporidhiana tulipitishe kwenye kamati hiyo, sasa wao hawajapita huko,” alisema. Mwigulu alibainisha kuwa UKAWA walishasema kuwa wiki hii haitaisha bila tukio lolote kutokea ndani ya Bunge na jambo hilo wamelifanya kwa kutoka nje ya Bunge ili kukwamisha mchakato huo. Mara baada ya Mwigulu kumaliza kuzungumza, Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samia Suluhu Hassan, alisema jambo hilo atalifikisha katika Kamati ya Uongozi ili kuangalia hatua za kuchukua. CHANZO: TANZANIA DAIMA 18.04.2014

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...