Thursday, 29 May 2014
HALIMA MDEE amvuruga Tibaijuka
Dodoma. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka jana alijikuta katika wakati mgumu wakati alipokuwa waziri wa kwanza kuhusishwa na tuhuma za ufisadi wa kutumia vibaya madaraka yake na lawama lukuki kuhusu kasoro za kiutendaji katika wizara anayoiongoza.
Mawaziri wengine wamekuwa wakiwekwa kitimoto kutokana na tuhuma za utendaji mbovu na udhaifu kwenye wizara zao, lakini hali ilikuwa tofauti jana wakati Waziri Kivuli wa Ardhi, Halima Mdee aliposoma hotuba ya kurasa 77 ya upinzani kuhusu makadirio na matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, huku kurasa 30 zikielekeza tuhuma kwa waziri huyo.
Miongoni mwa tuhuma zilizotolewa dhidi ya waziri huyo ni pamoja na kujinufaisha kupitia mgogoro wa ardhi katika eneo la Chasimba na kiwanda cha Saruji cha Wazo Hill jijini Dar es Salaam.
Mdee, ambaye pia ni mbunge wa Kawe, alimhusisha waziri huyo na ufisadi katika kazi ya utafiti uliofanywa na wataalamu wa masuala ya ardhi, uliogharimu Sh700 milioni. Tuhuma hizo zilimchanganya Waziri Tibaijuka kiasi kwamba wakati akitoa majibu alijikuta akitoka nje ya mada na kumshambulia Mdee, huku Spika Anne Makinda akimrudisha kila mara na kumtaka ajikite kwenye hoja na kuacha kushambulia wapinzani.
Waziri Tibaijuka pia alidai hotuba ya upinzani ilijaa uongo na kumtaka Spika Makinda kumchukulia hatua Mdee.
Akisoma maoni ya Kambi ya Upinzani bungeni jana, Mdee alisema utafiti huo ulikuwa na timu ya watu 140 kutoka taasisi mbalimbali ikiwemo, sekta binafsi na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Alisema waziri huyo anatuhumiwa kuingilia mchakato huo kwa kuingiza jamaa zake na taasisi ambazo ana uhusiano nazo kama sehemu ya kikosi kazi cha utafiti kwa jina la wataalamu washauri.
“Matokeo yake, Idara ya Uchumi ya UDSM ilitumika kama chambo huku kiasi kikubwa kikimrudia mwenyewe kwa mlango wa nyuma,” alisema Mdee.
“Ilifika hatua wataalamu walimsusia kazi waziri kutokana na kuwepo ujanja ujanja katika masuala ya fedha, hivyo kumlazimu waziri kujifungia na wasaidizi wake kukamilisha kazi iliyobaki.”
Kadhalika Mdee alimtuhumu Tibaijuka kwamba ana uhusiano na Taasisi ya Tanzania Women Land Access Trust (TAWLAT) ambayo ililipwa kiasi cha Sh300 milioni kutoka Manispaa ya Kinondoni kwa ajili ya kutoa elimu na kuendesha mazungumzo kwa diplomasia, kati ya viongozi na wananchi wa Chasimba kuhusu mgogoro wa ardhi.
“Licha ya kulipwa fedha hizo, TAWLAT haikufanya kazi yoyote ya uthamini katika eneo la Chasimba, badala yake aliyekuwa mkurugenzi wa upimaji, mthamini mkuu wa serikali pamoja na wataalamu wa wizara walikuja kuniomba niwatulize wananchi waliokuwa wanawarushia mawe kwa kuwa hawakuwa na imani na viongozi hao,” alisema Mdee.
Mdee, ambaye pia ni mbunge wa Kawe (Chadema), aliitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuichunguza TAWLAT kuhusu ushiriki wake aliosema una shaka katika kazi kadhaa za Wizara ya Ardhi.
Mdee alisema awali Profesa Tibaijuka alikubaliana na wananchi katika mikutano mbalimbali kwamba watalipwa fidia ya Sh15,000 kwa kila mita ya mraba, lakini baadaye alifanya kikao kingine na kuwageuka.
“Kikao hicho cha pili kiliwahusisha diwani wa Kata ya Bunju, kamati ya wananchi na mwenyekiti wa Mtaa wa Basihaya na Tibaijuka alibadili kauli yake na kusema wananchi hawatalipwa kiasi hicho cha fedha, bali watapewa Sh5,000 kama kifuta jasho.”
Alisema kauli hiyo ya waziri ilikuwa ni tofauti na maneno yake kwenye barua yake yenye kumb CBA 171/312/01.C kwenda kwa waziri mkuu, ambayo pamoja na mambo mengine ilieleza kuwapo kwa mahitaji ya Sh69 bilioni kwa ajili ya fidia, ikiwa ni Sh15,000 kwa mita za mraba na kulipwa Sh5,000 kwa mita na kuhoji kilipo kiasi cha Sh10,000.
“Kwa mujibu wa tathmini iliyofanyika, kaya zilizotakiwa kupewa viwanja mbadala ni 4,096, iweje viwanja ambavyo wizara inataka kuvilipia ni 4,500, viwanja vilivyosalia 404 vya ziada ni mali ya nani?”
Ajibu mapigo
Akijibu tuhuma hizo, Profesa Anna Tibaijuka, alisema: “Mheshimiwa spika, kanuni ya 56 inakataza mbunge kusema uongo, lakini hapa kuna mbunge amesema uongo.”
Huku akikumbushwa kutolumbana na wapinzani, Waziri Tibaijuka alijikuta akiwaambia wananchi wa Jimbo la Kawe kwamba wasimchague tena Mdee akidai ‘itakula kwao.’
Alisema Mdee anasema kuna ‘dili’ anafanya katika mgogoro wa Chasimba wilayani Kinondoni.
“Sifanyi dili katika mgogoro wa eneo la Chasimba. Nafanya kazi kwa uadilifu, wala sina personal interest (masilahi binafsi) kuhusu eneo hilo. Kinachozungumzwa na Mdee ni propaganda, lakini hawezi kunizuia kumaliza mgogoro huo,” alisema Tibaijuka.
Alisema mgogoro wa Chasimba karibu utamalizika na wananchi kutalipwa fidia, lakini mbunge wao anataka kuvuruga katika hatua waliyofikia kwa maslahi binafsi ya kisiasa.
Akionyeshwa kukasirishwa na tuhuma za Mdee, Tibaijuka alisema amefikia hatua ya kuiba barua ya kiofisi ambayo yeye alimwandikia Waziri Mkuu Mizengo Pinda na kuiweka katika hotuba yake.
“Kwa hiyo Mheshimiwa Spika nakukabidhi barua yangu na hotuba yake ili muone hatua zinazoweza kuchukuliwa,” alisema Tibaijuka.
Alisema kambi ya upinzani hawako pamoja kwani wakati kiongozi wa kambi hiyo, Freeman Mbowe akilaumu ujenzi holela katika miji yetu, Mdee anataka eneo la Chasimba libaki vilevile wakati limejengwa kiholela.
Kuhusu TAWLAT, Waziri Tibaijuka alisema: “Hizi tuhuma za rejareja lazima tuzijibu. Shirika la TAWLAT liliundwa nikiwa UN-HABITAT kwa ajili ya kuwasaidia wanawake kupata ardhi mijini. Nalilea shirika hilo na lipo Kenya (KEWLAT), Uganda (UGLAT), Msumbiji (MUZLAT) na Ghana (GHAULAT).”
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment