Thursday, 17 April 2014
ASASI ZATAKA BUNGE LIVUNJWE
IMEELEZWA kuwa hakuna sababu ya kuendelea na Bunge Maalumu la Katiba, kama rasimu ya pili iliyopelekwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba inadhihakiwa na kudharauliwa.
Hayo yalisemwa jana katika tamko la pamoja la asasi zipatazo 500, zilizokuwa zikieleza masikitiko yake kuhusu mwenendo mzima wa bunge hilo mpaka lilipofikia sasa.
Akisoma tamko hilo mbele ya waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Umoja wa Azaki hizo, Irinei Kiria, alisema bunge hilo linapaswa kujua kwamba halipo juu ya mchakato bali ni sehemu tu tena ya pili toka hatua ya mwisho ya mchakato ambayo itakuwa ni kura ya maoni.
“Toka awali msimamo wa Azaki umekuwa ni kupatikana kwa katiba ya wananchi yenye malengo mapana kwa manufaa ya nchi na vile vile katiba ya kudumu kwa muda mrefu na wala si katiba ya kusaidia makundi machache katika jamii ya Watanzania tena wakati mwingine kwa malengo ya muda mfupi kabisa.
“Vilevile Azaki tumekuwa na msimamo kwamba katiba itakayopatikana ijidhihirishe kimuundo kwamba si ya kukidhi masilahi ya watawala bali ionyeshe kwamba inatoa majibu ya kero na matatizo yaliyodumu kwa muda mrefu kama vile ufisadi, kutowajibika kwa viongozi na watendaji wa umma, kukosekana kwa maadili ya viongozi, umaskini, ukiukwaji wa haki za binadamu, uchumi mbovu na kero za Muungano.
“Kwa bahati mbaya tumebaini kuwa taswira iliyopo sasa hasa katika Bunge Maalumu la Katiba inafifisha matamanio yetu ya Tanzania mpya kwa kuwa haionyeshi dalili zozote nzuri za kupata katiba ya wananchi,” alisema mwenyekiti huyo.
Mbali na kudharauliwa kwa maoni ya tume ambayo ndiyo maoni ya wananchi, asasi hizo zimesema majadiliamo bungeni yamekosa utashi wa utaifa, yamepoteza moyo wa maridhiano na kuheshimiana, badala yake wanaona ubabe, ubaguzi, vijembe, vitisho, nguvu ya wingi wa watu na vyama.
Pia ni malumbano yasiyo na tija na yaliyopoteza muda na rasilimali za Watanzania. Malumbano hayo ni kama vile ya kura za siri au za wazi wakati siku zote inafahamika kwamba mpiga kura anatakiwa kujengewa mazingira ya kuchagua kile anachokiridhia na wala si kwa kumridhisha mtu mwingine.
Kumekuwepo na lugha ya vitisho na ubaguzi kwa wananchi na hata kwa wajumbe wa Bunge la Katiba wenye misimamo huru na hasa kwa wale wanaosimama na kutetea maoni ya wananchi.
“Vitisho hivi havitoki tu ndani ya wajumbe wa Bunge la Katiba wenyewe bali hata kutoka kwa viongozi mbalimbali wa nchi. Vitisho hivyo ni pamoja na kauli ya Rais wakati analihutubia Bunge ambako aliwaambia wajumbe wa Bunge kuwa kupitisha Muundo wa Muungano ambao wananchi wameupendekeza kwenye rasimu inayojadiliwa bungeni itatoa mwanya kwa jeshi kupindua nchi.
“Kauli hii imeendelea kurudiwa na viongozi mawaziri katika maeneo mbalimbali akiwemo Waziri William Lukuvi aliyekaririwa akiwaambia waumini wa dini moja mjini Dodoma kuwa endapo mapendekezo ya rasimu inayojadiliwa bungeni juu ya muundo wa Muungano yatapita tambueni nchi itatawaliwa na jeshi.
“Kauli nyingine ya vitisho ni ile inayoelekezwa kwa wajumbe wanaoitetea rasimu hii ya wananchi, wamekuwa wakiambiwa kuwa kupitisha mapendekezo ya rasimu hii, hasa muundo wa shirikisho ni kuvunja muungano na kumrudisha sultani kwa upande wa Zanzibar,” alisema.
Kushambuliwa Warioba Binafsi
Aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko, Humphrey Polepole, alisema wanawashangaa watu ambao wamekuwa wakimshambulia Warioba binafsi wakati kazi ya kukusanywa maoni ilifanywa na jumla ya wajumbe 30, 15 kutoka Bara na 15 kutoka Visiwani Zanzibar.
Badala yake Polepole alisema ni vyema sasa hivi wakamuacha Warioba akapumzika kwani kutokana na walivyomsakama kama angeenda kufanyiwa uchunguzi wa afya basi huenda akawa amepunguza kilo kadhaa.
Hata hivyo mjumbe huyo alisema watu wanapaswa kuelewa kwamba katiba inapaswa kuandikwa kwa majadiliano, makubaliano na maridhiano na suala la kupiga kura linakuja mwishoni kabisa.
Polepole alisisitiza kwamba waliyoayaandika kwenye rasimu ya pili ndicho walichokisema wananchi na kwamwe hawapo tayari kubadili ukweli huo.
UKAWA kutoka nje ya Bunge
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Hellen Kijo Bisimba, alisema kitendo cha UKAWA kutoka nje ya Bunge si sahihi kwani kitapunguza nguvu ya kudai yale wanayoamini ndiyo sahihi.
Badala yake aliwataka warudi ndani na washikamane na wadau wengine, ikiwemo kulivunja bunge hilo ambalo mpaka sasa tayari limepoteza fedha nyingi za walipa kodi.
Pia alisema wanasikitishwa sana na kupotoshwa kwaa baadhi ya taarifa za tume ambayo ilisheheni wataalamu wa maeneo mbalimbali.
Kwa mujibu wa Bisimba watu hao walitaka utafiti wa aina gani ili wajue ndio maoni ya kweli ya wananchi, kwani kama ni suala la idadi mbona wao wapo wajumbe takriban 600 na wameaminiwa katika kupitia rasimu hiyo.
Rai yao kwa Bunge la Katiba
Asasi hizo zimelitaka Bunge hilo kujua kwamba halina mamlaka ya kubadili mambo ya msingi katika Rasimu ya Katiba kwa madai kwamba linakosa uhalali huo kwanza kutokana na muundo wa mchakato wa uandaaji wa Katiba hapa nchini.
Wakifafanua zaidi kuhusu hili, walisema muundo umekuwa shirikishi na kuundwa kwa tume kwa ajili ya kukusanya maoni ya wananchi tayari kumelipunguzia Bunge madaraka makubwa.
Kwa maana hiyo Bunge hili halina mamlaka ya kubadili rasimu hii zaidi ya kujadili, kuboresha na kuongeza masharti ya mpito, sheria ambayo ipo katika Kifungu cha 25 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83.
CHANZO: TANZANIA DAIMA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment