KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amewataka Watanzania kufahamu kuwa hakuna chama cha upinzani chenye lengo la kuvunja Muungano.
Alisema maneno yanayoelezwa na wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni njama ya kudhoofisha msimamo wa kuwapo serikali tatu.
Aliyasema hayo juzi alipowahutubia wakazi wa Jiji la Tanga kuhusu mabadiliko ya rasimu ya katiba mpya katika viwanja vya Tangamano alipokuwa timu ya viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kuwataka wakazi wa jiji hilo kukataa hadaa zinazofanywa ili kukanyaga rasimu waliyoitolea maoni.
Alisema Rais Jakaya Kikwete anawarubuni wananchi anaposema wanaotaka serikali tatu wana lengo la kuvunja Muungano, na kusisitiza kuwa hakuna chama chochote cha upinzani ambacho kinataka Muungano uvunjike kwani kila mwananchi anahitaji maendeleo na hizo ni siasa.
Dk. Slaa ambaye sasa ni Mwenyekiti wa Ukawa nje ya Bunge Maalumu la Katiba, alisema Rais Kikwete alipotoka wakati akihutubia Bunge Maalumu la Katiba kwa kuiponda katiba na kumdhalilisha aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
“CHADEMA, Cuf, Nccr-Mageuzi na Watanzania hakuna anayetaka Muungano uvunjike, bali kinachofanywa na CCM ni kuwachonganisha kwa wananchi ili waonekane ni maadui wa Muungano,” alisema Dk. Slaa.
Alisema inasikitisha kuona baadhi ya wajumbe kutoka Zanzibar ndani ya Bunge hilo wakidanganywa kuahidiwa kupewa fedha za kuwasomesha ili waunge mkono msimamo wa kupiga kura serikali mbili jambo ambalo ni kinyume cha malengo ya uwakilishi wao kwa Watanzania.
“Chini ya umoja wa Ukawa, wanachofanya ni kutetea maoni ya wananchi yaliyotolewa kwenye tume ya katiba kwa kuwa Tanzania ni nchi ya wote na hakuna ambaye akifa atazikwa nje ya nchi hii, hivyo lazima kutetea maslahi ya wananchi,” alisema Dk. Slaa.
No comments:
Post a Comment