WIKI moja baada ya Mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM), kutoa kauli inayofananishwa na ile ya hayati Baba wa Taifa, Julius Nyerere, ya kwamba chama hicho si mama yake, uongozi wa Mkoa wa Shinyanga umemjia juu ukidai amekejeli chama na sasa unamwandalia zengwe kumng’oa.
Katika mahojiano na waandishi wa habari nje ya Ukumbi wa Bunge mjini Dodoma wiki iliyopita, Lembeli alisema kuwa liwalo na liwe lakini hataacha kuitetea Serikali ya Tanganyika.
Alisema kuwa huo ni msimamo wake na utabaki kuwa historia ambayo haikarabatiwi huku akiwataka wenzake wenye msimamo kama huo kuacha woga, akisema kuwa wenye kumshughulikia ni wapiga kura wake endapo atakwenda kinyume cha matakwa yao.
Kauli hiyo imeonekana imewaibua viongozi wa CCM Mkoa wa Shinyanga ambapo jana Mwenyekiti wa mkoa, Khamis Mgeja, Mjumbe wa NEC, Boniface Butondo, Katibu wa mkoa, Adam Ngalawa na Katibu Mwenezi wa mkoa, Emmanuel Mlimandago, walikutana na waandishi wa habari mjini Dodoma kulaani kauli hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Mlimandago alisema kauli ya Lembeli wanailaani kwa vile inaonyesha dharau kwa chama chake.
“CCM Mkoa wa Shinyanga kimelaani vikali kauli ya Lembeli aliyoitoa kwenye vyombo vya habari akisema CCM si mama yake.
“Tunaomba ieleweke kwamba, CCM haina tatizo na msimamo wa mbunge huyo kuhusu serikali moja, mbili, tatu au serikali nne na hata Serikali ya Tanganyika.
“Tatizo letu kubwa ni kauli hiyo aliyoitoa, kwani alipoitolea hapakuwa mahali pake na haihusiki na utashi wake binafsi alionao katika Bunge la Katiba, kwa kifupi kauli hiyo ina ukakasi na inakinajisi chama chetu,” alisema.
Alisema kuwa jambo la kushangaza ni kwamba Lembeli amekuwa akilitumia vibaya jina la Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Nyerere, kwani anajifananisha naye wakati hana sifa zozote zinazofanana.
“Hafanani na Baba wa Taifa kwa sababu Mwalimu Nyerere alipokuwa akizungumzia suala linalohusu mustakabali wa chama na taifa kwa ujumla, alikuwa akitumia vikao na si kuropoka au kuzungumza hovyo,” alisema Mlimandago.
Pamoja na hayo, alisema mwenendo wa Lembeli katika chama unatia shaka kwa vile amekuwa na kawaida ya kukikosoa bila kufuata utaratibu.
“Lakini tunapenda Lembeli atambue kwamba, umaarufu wake umetokana na CCM kwani kabla ya mwaka 2005 hakukuwa na Watanzania wengi waliokuwa wakimfahamu kama ilivyo sasa.
“Kwa hiyo, kama kweli CCM si mama yake, ni vema akatueleza mama yake ni nani kisiasa ili aweze kumfuata huko aliko,” alisema.
Kauli ya Lembeli
Katika kauli yake, Lembeli alisema baadhi ya wajumbe ni waoga na wanafiki kwa kuogopa kusimamia kile wanachokiamini.
“Historia haikarabatiwi, mimi naweza kufa au kuadhibiwa na chama changu kutokana na msimamo huu lakini histori itaandikwa.
“Pale Ikulu si kuna picha ya hayati Oscar Kambona, huyu si alifungwa kwa makosa ya uhaini mbona picha yake haikuondolewa katika viongozi wa historia ya nchi hii?” alihoji.
Lembeli alihadi kuwa wamsubiri watamuona wakati wa mjadala wa pamoja bungeni huku akitamba kwamba hatabadili msimamo hata kama unakinzana na wenzake wa CCM.
“Sina wa kumfurahisha zaidi ya wapiga kura wangu, hawa ndio wenye uwezo wa kunishughulikia endapo nitaunga mkono jambo ambalo litakuwa kinyume na wao.
“Mimi ndiye Lembeli na nitabakia kuwa hivyo, ndiyo maana nilikuwa nataka itumike kura ya siri ili kuhifadhi uhuru wa mawazo yetu. Nyerere alituambia kuwa wananchi wanataka mabadiliko na wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM,” alisisitiza.
Lembeli aliwataka wajumbe wenzake kuacha woga wa kufungwa na misimamo ya vyama au makundi yao kwani hata Rais Jakaya Kikwete aliwaambia kuwa akili za kuambiwa wachanganye na za kwao.
Chanzo cha Habari hii ni Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment