Saturday, 19 April 2014
Polisi wavaa joho la ccm
Yatangaza vita kuusambaratisha Umoja wa UKAWA
Slaa asema Pasaka yao imo kwenye mapambano
MKAKATI wa kupambana na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) nje ya Bunge, ambao awali ulikuwa ukifanywa na viongozi na makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) nje na ndani ya Bunge, sasa umehamishiwa mikononi mwa Jeshi la Polisi ambalo limeapa kuusambaratisha umoja huo, Tanzania Daima Jumapili limebaini.
Hali hiyo imebainika jana baada ya jeshi hilo kutangaza kupiga marufuku mikutano na shughuli zote za vyama vya siasa, ikiwemo za UKAWA si tu kwa Visiwani Zanzibar bali pia kwa Tanzania Bara.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili jana, Msemaji wa Jeshi hilo nchini, Advera Senso, alisema wamezuia mikutano na shughuli za hadhara za vyama vya siasa baada ya kubaini kuwapo viashiria vya uvunjifu wa amani katika mikutano hiyo.
“Polisi tukishapata taarifa kama kuna mkutano unafanyika au utafanyika, tunachofanya ni kuangalia hali ya usalama na kama tukibaini viashiria vya uvunjifu wa amani ndipo tunakataza kufanyika kwa mikutano hiyo. Na hiki ndicho kilichotokea Zanzibar na viashiria hivyo pia vipo Tanzania Bara,” alisema.
Alipoulizwa ni viashiria gani walivyobaini vya uvunjifu wa amani nchini kwa sasa, msemaji huyo wa Polisi alikataa kuvitaja kwa sababu alizodai kuwa ni za kiusalama.
“Siwezi uvitaja ni viashiria gani kwani hupaswi kujua hayo ni mambo ya kipolisi na yenye taaluma yake kama ilivyo kwenu katika vyombo vya habari,” alisema.
Kwa mujibu wa Polisi, agizo la kuzuia shughuli na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, litaendelea hadi pale watakapojiridhisha kwamba hali ya usalama ni shwari.
Hata hivyo habari za kiuchunguzi ambazo gazeti hili limezipata, zilisema kuwa mkakati wa kutumia Polisi kupambana na UKAWA umetokana na shinikizo la viongozi wa serikali, hasa baada ya kundi hilo kuamua kususa vikao vya Bunge Maalumu vinavyoendelea mjini Dodoma.
Kwa hali hiyo, kundi hilo sasa halitaweza kufanya mikutano ya hadhara na kuwaeleza wananchi kinachoendelea bungeni, badala yake serikali imeweka mkakati wa kuwataka warejee kwenye meza ya majadiliano na kisha warejee bungeni.
Duru za siasa zinasema kuwa CCM wamebaini bila kuusambaratisha UKAWA ni vigumu kwa chama hicho tawala kutimiza azima yake ya kuhakikisha mfumo wa serikali mbili wanaoutaka unapitishwa, tofauti na serikali tatu zilizopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba iliyokusanya maoni ya wananchi kutaka serikali tatu.
Dk. Slaa awalipua Polisi
Wakati polisi ikivaa joho la CCM kupambana na UKAWA, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, amesema kuwa kinachofanywa na polisi ni maagizo ya serikali, lakini kamwe mkakati huo hauwezi kufanikiwa.
Alisema kazi ya polisi si kuzuia bali ni kutoa ulinzi na kuwakamata watakaobainika kusababisha vitendo vya uvunjifu wa amani kwenye mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.
“Mimi nawashangaa polisi kukubali kutumiwa na CCM. Watuambie tahadhari ya hali ya hatari imeanza lini?” alihoji Dk. Slaa.
Hata hivyo alisema uamuzi wa CCM kutumia polisi umeongeza kasi ya UKAWA kudai Katiba bora, kwani hali hiyo inawafanya hata wananchi wa kawaida kujiuliza kulikoni hadi polisi watumike kudhibiti wapinzani.
“Polisi wanatusaidia, wanafanya wananchi wajiulize na wajue kwamba CCM inatumia nguvu kupitisha hoja zao kwenye Katiba Mpya.
“Hizi ni dalili za ukombozi, unaweza kufanya kila kitu, kutisha kupiga watu, lakini ukombozi ukishafika, umefika, huwezi kuuzuia, sawa na giza, ukiona giza nene unajua mwanga unakuja.
“Leo ni Pasaka, lakini hatuna Pasaka njema, sherehe yetu ya Pasaka imo kwenye mapambano, kila Mtazania ajue haya ni mapambano,” alimaliza kusema Dk. Slaa.
Juzi UKAWA walisema hawatarudi bungeni na badala yake wataanza mikutano ya hadhara nchi nzima kuwaeleza wananchi juu ya hila za CCM na washirika wake kutaka kuhodhi mchakato wa uandikaji wa Katiba mpya.
UKAWA wamesema katika mikutano hiyo watazisambaza ‘CD’ zinazomuonyesha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, akiwa katika Kanisa la Methodist, mkoani Dodoma akiwaeleza waumini wakatae muundo wa serikali tatu.
Walisema kwenye CD hizo, Lukuvi, anaonekana akiwaambia wananchi iwapo wataridhia muundo wa serikali tatu, jeshi litachukua nchi na Zanzibar itaingia katika utawala wa Kiislamu.
Walitangaza uamuzi huo baada ya kutoka ndani ya Bunge kwa madai ya kuchoshwa kusikiliza matusi, ubaguzi na kauli za chuki zinazotolewa na wajumbe kutoka CCM bila viongozi wakubwa kukemea.
UKAWA waliweka msimamo kuwa hawatarejea bungeni mpaka watakapoketi kwenye vikao vya maridhiano ambavyo pia watakwenda na masharti yao, mojawapo ni rasimu ya Tume ya Warioba ndiyo iwe msingi wa majadiliano.
Masharti mengine ni kukaa kwenye meza ya maridhiano na viongozi wa serikali na CCM, kusiwepo matusi, ubaguzi na kauli za chuki.
chanzo:Tanzania daima
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment