Social Icons

.

Saturday, 26 April 2014

Viwango, kasi vya Sitta vimepwaya

MWENYEKITI wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, ameliahirisha Bunge hilo juzi huku akijitetea kwa hoja dhaifu kuhusu tuhuma za kushindwa kwake kusimamia nidhamu kwa wajumbe.Tangu kuanza kwa mjadala wa sura mbili za rasimu ya katiba, yaani sura ya kwanza na sita, wajumbe wengi wamekuwa wakitumia muda mwingi kuporomosha matusi na vitisho vya kila aina kwa wenzao wanaotaka muundo wa serikali tatu.Matusi na vitisho hivyo vinaudhi, vinakera na havikustahili kusikika masikioni mwa jamii iliyostaarabika, pia katika watu wa taifa lenye amani, utulivu na kuheshimiana kwa muda mrefu kama Tanzania.Kwa bahati mbaya, kauli hizo chafu zilitumika bila Mwenyekiti wa Bunge wala Makamu wake kuingilia kati kuwakemea waliokuwa wakifanya hivyo na hata wale waliotakiwa kufuta kauli zao lakini wakakataa, bado kiti kilishindwa kuwachukulia hatua yoyote.Lakini katika hatua ya kushangaza wakati akiahirisha Bunge Maalumu, Sitta alijitetea akisema si kweli kwamba aliwafumbia macho watukanaji na watoa vitisho, bali alishauriana na makamu wake, Samia Suluhu Hassan, wakaamua kuwaacha ili jamii iwaone.Kwa mujibu wa Sitta, kama wangetumia kanuni kuwabana watukanaji, basi wako ambao walipaswa kutolewa nje, tena kwa kubebwa juu kwa juu na askari wa Bunge, jambo alilodai kuwa lingeweza kusababisha vurugu za watu kupigana.Kwa utetezi huu, lazima tutofautiane na Sitta, kwa sababu hoja zake ni za kitoto sana, wakati chombo anachokiongoza kina hadhi kubwa ndani na nje ya nchi.Kushindwa kwake kuwachukulia hatua wahusika, amelifanya Bunge lote kama taasisi kudhalilika, wajumbe wameonekana watu wa hovyo mbele ya umma.Kanuni za kumsaidia kutoa adhabu zipo lakini hazikutumika. Huku ni kupwaya, ni woga, ni unafiki kwa sababu huyo siyo Sitta wa kasi na viwango tuliyemfahamu wakati wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Tunasema hivyo kwa sababu inashangaza kuona Sitta na viongozi wengine wengi wa CCM walikuwa mstari wa mbele kulalamika kwamba kuna baadhi ya wajumbe wa upinzani waliwakashfu waasisi wa taifa, hayati Julius Nyerere na Abeid Aman Karume, lakini hatukuona wakiadhibiwa.Wajumbe takriban wote wa CCM walimtusi aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume, Jaji Joseph Warioba ndani na nje ya Ukumbi wa Bunge, tena kwa maneno makali, lakini si Sitta wala Samia aliyeguswa na matusi hayo.Kama viongozi hawa walishindwa kuzisimamia kanuni za Bunge walizojiwekea wenyewe badala yake wanasema waliwaacha watukanaji ili jamii iwaone, basi hawana budi kujiengua kwenye madaraka yao.Kinachomsababisha Sitta ashindwe kulimudu Bunge Maalumu la Katiba ni kwa sababu naye ni sehemu ya mashabiki na wakereketwa wa muundo wa serikali mbili unaopigiwa chapuo na CCM, hivyo wakati mwingine anajikuta akifurahia matusi na vitisho vinavyoelekezwa kwa wajumbe wanaounga mkono serikali tatu.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...