Social Icons

.

Monday, 16 June 2014

Bajeti ya Upinzani yaonyesha Mwanga ya serikali yawe maigizo

WAKATI serikali ikishindwa kubainisha vyanzo vipya vya mapato, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imeainisha maeneo nane yatakayoliwezesha taifa kupata sh trilioni 6.194. Mbali na kutoa vyanzo hivyo vipya, bajeti mbadala ya upinzani inaonyesha taifa litakusanya na kutumia sh trilioni 21.7. Vyanzo hivyo na matumizi hayo vilibainishwa jana bungeni na Waziri kivuli wa Fedha, James Mbatia, alipokuwa akisoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka 2014/2015. Mbatia aliyataja maeneo hayo na kiasi cha fedha kitakachopatikana ni kudhibiti ukwepaji wa kodi na udanganyifu (sh trilioni 1.9), kuongeza ufanisi TRA (bilioni 708.1), kudhibiti misamaha ya kodi (trilioni 1.3), kuongeza ufanisi wa bandari (trilioni 1.4), pesa fasta, tozo la asilimia 15 kwenye faida ya wakala wa kampuni za simu (bilioni 268.8). Tozo ya asilimia 1 ya manunuzi yote ya nje na tozo ya asilimia 0.5 ya mauzo yote ya nje (sh bilioni 226.1), mrabaha wa asilimia 5 kwenye uvuvi wa samaki-bahari kuu (sh bilioni 14) na marekebisho ya kodi sekta ya misitu (sh bilioni 220.4). Mbatia alisema kuwa katika bajeti hiyo mbadala, mapato ya ndani yatakuwa ni asilimia 84.38 ambayo ni sawa na sh bilioni 18.372 ambapo mapato ya kodi (TRA) ni sh trilioni 17.2, mapato yasiyo na kodi sh trilioni 1.099, mapato ya halmashauri sh bilioni 458.4, mikopo, misaada ya kibajeti sh bilioni 922 na mikopo na misaada ya miradi ya maendeleo sh trilioni 2. Jumla ya mikopo na misaada ya nje sh trilioni 2.9 ambapo jumla ya mapato yote ni sh trilioni 21.7. Mbatia alibainisha kuwa matumizi ya kawaida ni sh trilioni 12. 4, deni la taifa  sh trilioni 4.1, mishahara sh trilioni 6, matumizi mengineyo   sh trilioni 2.2, wizara sh trilioni 1.8, mikoa sh bilioni 45.8, halmashauri sh bilioni 366.8, matumizi ya maendeleo sh trilioni 9.2 ambapo fedha za ndani ni sh trilioni 6.3 na fedha za nje  ni sh trilioni 2.9. Waziri huyo kivuli alibainisha kuwa vipaumbele vya kambi hiyo ni ni utawala bora, elimu, kilimo, afya, miundombinu, nyumba na makazi, michezo na sanaa, ajira (kukuza uchumi vijijini) na ulinzi wa rasilimali za taifa – wanyamapori, misitu, ardhi, uoto wa asili, maziwa, mito, bahari pamoja na mazao yake. Alibainisha kuwa kuimarisha utawala bora kutachangia kuboreka kwa uendeshaji wa shughuli za serikali na taasisi zake katika ngazi zote kwa kuzingatia sheria, kanuni, miiko na miongozo inayowekwa. Azungumzia deni la taifa Kuhusu deni la taifa Mbatia, alisema limeongezeka kwa kasi kubwa hali ambayo inahatarisha ustawi wa taifa kama halitasimamiwa kwa umakini na haraka kwakuwa linaonekana kuendelea kuongezeka kwa sababu serikali inatarajia kukopa zaidi ya sh trilioni 4. Alisema hadi kufikia Machi 2014, deni la taifa lilifikia sh trilioni 30 ikilinganishwa na sh trilioni 23.6 Machi 2013 ambapo ni ongezeko la takribani trilioni 7 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 29 kwa kipindi cha mwaka mmoja tu. Alibainisha kuwa ongezeko la mikopo ya takribani shilingi trilioni 7 kwa mwaka mmoja tu, halijawahi kutokea katika historia ya Tanzania ambapo ni sawa na bajeti nzima ya mwaka 2008/9 ambayo ilikuwa ni shilingi trilioni 6.839. Alisema ni vigumu serikali kulipa deni hilo kwakuwa katika uchumi unaokua kati ya asilimia 6.5 hadi 7 kwa mwaka, ni vigumu kulipa deni linalokua kwa wastani wa asilimia 15 na 30 kwa mwaka. Tofauti ya bajeti ya serikali na upinzani Bajeti ya upinzani inaendelea kusisitiza kushusha kiwango cha  tozo ya kodi ya mapato ya ajira kwa wafanyakazi (PAYE) hadi kufikia asilimia 9 ilhali ya serikali inatoza asilimia 12. Bajeti ya upinzani imeainisha vyanzo vipya vya mapato ya ndani, na hivyo  kuwa inayojitegemea kwa asilimia 84.38, ilhali bajeti ya serikali ni  tegemezi kwa asilimia 36.4 kutokana na kukopa kwa kiwango kikubwa na hivyo  kuongeza deni la taifa. Bajeti mbadala, mapato ya ndani ni asilimia 34.55 ya pato la taifa  wakati bajeti ya serikali, mapato ya ndani ni asilimia 23 ya pato la taifa. Bajeti ya upinzani inalenga kupunguza misamaha ya kodi hadi kufikia asilimia 1 ya pato la taifa ili kuongeza mapato ya ndani ilihali ya serikali imetaja tu azma ya kupunguza misamaha ya kodi. Upinzani unalenga kutekeleza kikamilifu  miradi ya maendeleo kwa kutenga asilimia 42.67 ya bajeti yote kugharamia miradi ya maendeleo wakati asilimia 22 ya bajeti yote ya serikali inakwenda kulipa deni la taifa na asilimia 67.5 ni  matumizi ya kawaida. Hivyo miradi ya maendeleo haijapewa kipaumbele. Bajeti ya upinzani itakusanya mapato kutoka kwenye vyanzo ambavyo havimuumizi mwananchi wa kawaida wakati bajeti ya serikali imelenga kukusanya mapato kutoka katika bidhaa zinazotumiwa kila siku na wananchi kama vile vinywaji, na hivyo kuwaongezea ugumu wa maisha. Bajeti ya upinzani inaonyesha matumizi ya kawaida ni asilimia 57.33 tu ya bajeti yote wakati ile ya serikali ikiainisha matumizi ya kawaida ni asilimia 67.5

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...